Thursday 20 October 2016

Polisi yauwa majambazi Dar


WATU sita wanaotuhumiwa kuwa majambazi hatari, wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha.
Mkondya alisema wamepata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), tawi la Barabara ya Nyerere, ambaye angepita katika barabara hiyo kwenda mkoani Morogoro.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.
“Majambazi wawili wakiwa na bastola walishuka katika gari hilo. Baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa polisi, walianza kufyatua risasi kwa askari wakitumia bastola na wenzao waliokuwa wamejaa kwenye gari yao walianza kushuka huku wakifyatua risasi kuelekea kwa askari,” alisema Kaimu Kamanda Mkondya.
Alisema kutokana na hali hiyo, askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la tukio.
Miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi.
Katika tukio lingine la Oktoba 17, mwaka huu saa 2:00 usiku katika maeneo ya Tegeta Masaiti, watuhumiwa watatu wa ujambazi wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki aina ya Fekon yenye namba MC370 BEY, wakiwa na bunduki aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, walivamia duka la Abdallah Juma (46), mkazi wa Tegeta na kupora fedha za mauzo na kuiba vocha za mitandao mbalimbali, ambazo thamani yake haijafahamika.
“Polisi baada ya kupata taarifa waliwafukuza majambazi hao, walipoona wanakaribiwa na askari, walitupa chini begi walilokuwa nalo na kutelekeza pikipiki yao kisha kukimbia, begi lilipopekuliwa lilipatikana na silaha hiyo,” alisema.
Aidha, wananchi wenye hasira waliendelea kuwakimbiza majambazi hao na kumuua mmoja huku wengine wakikimbilia kusikojulikana. Katika hatua nyingine, Mkondya alisema wamekamata watuhumiwa wawili wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu wakiwa na pikipiki moja na funguo bandia 75.
Alisema watuhumiwa hao, Ally Makwega (53) mkazi wa Tandika na Fabian Greyson (39) mkazi wa Yombo walikamatwa Oktoba 4, mwaka huu saa 6:00 usiku.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pikipiki yenye namba MC292 AMD aina ya Boxer rangi nyekundu, wanayoitumia kufanya uhalifu, wakiwa na funguo bandia 75 ambazo huzitumia katika kuvunja nyumba mbalimbali ya biashara za kulala wageni, maghala ya kuhifadhia bidhaa na maduka.
Baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa maghala na kuiba katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. Mkoani Tanga, Anna Makange anaripoti kuwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni mkazi wa Kata ya Sindeni wilayani Handeni, ameuawa kwa risasi na mjomba wake mwenye umri wa miaka sita wakati walipokuwa wakichezea bunduki aina ya gobori nyumbani kwao.
Tukio hilo la kusikitisha, limetokea katika Kijiji cha Kweditilibe, wakati watoto hao ambao ni ndugu wa familia moja walipokuwa wakichezea bunduki hiyo inayomilikiwa na baba wa mtoto aliyeuawa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha jana kutokea kwa mauaji hayo na kusema yalifanyika Oktoba 17, mwaka huu saa 12:30 jioni.
“Siku hiyo ya tukio, mmiliki wa gobori hilo ambaye ndiye baba mzazi wa mtoto aliyeuawa, inadaiwa alikuwa ameliweka hapo nyumbani na ndipo hao watoto wakaingia na kulichukua kwa ajili ya kulitumia wakati wakicheza nje na ndipo mtoto ambaye inadaiwa ni mjomba wa marehemu alipomfyatulia risasi mwenzake na kusababisha kifo hicho,” alisema Kamanda Wakulyamba.
Kamanda Wakulyamba alisema mmiliki wa gobori hilo ambaye ni mzazi wa marehemu, anaendelea kutafutwa na polisi kwa kuwa hakuweza kupatikana baada ya mauaji hayo na kwamba uchunguzi kuhusu tukio hilo bado unaendelea.
Katika tukio jingine lililotokea kwenye Kata ya Mazinde wilayani Korogwe, mfugaji Maliki Kilimbo (18) amejeruhiwa kwenye goti lake la mguu wa kushoto kwa kupigwa risasi wakati akilisha mifugo ndani ya shamba la mwekezaji. Kamanda Wakulyamba alisema uhalifu huo ulifanyika Oktoba 17, mwaka huu saa 12:30 jioni wakati mfugaji huyo alipoingiza mifugo kwenye shamba la mkonge, mali ya Kampuni ya Toronto.
“Kilimbo alijeruhiwa kwa risasi ya bunduki aina ya gobori na mlinzi wa Kampuni ya Toronto aitwae Benjamin Mgiriki.... upelelezi kuhusu tukio hili bado unaendelea,” alisema.
Mkoani Rukwa, Peti Siyame anaripoti kuwa wananchi katika Kijiji cha Legezamwendo wilayani Sumbawanga, wamemuua kwa kumkata kata kwa mapanga mkazi wa kijiji cha Mkusi, Erick Nkrukizi (30) na kuuchoma moto mwili wake baada ya kumkamata akitaka kuumua mwanamke, Nkundi Masingija.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema mauaji hayo yalifanyika Oktoba 19, mwaka huu, saa mbili usiku, baada ya kundi la watu hao, kufanya mauaji hayo. Watu hao hawajafahamika. Uchunguzi wa polisi unaendelea ili kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.
Share:

Wednesday 19 October 2016

Waziri Mkuu aagiza wanaoharibu mazingira kuchukuliwa hatua


Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA ameuagiza uongozi wa mkoa wa LINDI kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria
Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA ameuagiza uongozi wa mkoa wa LINDI kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wanaoharibu mazingira kwa kufyeka na kuchoma moto misitu. 
Waziri Mkuu MAJALIWA ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya RUANGWA kwenye mikutano ya hadhara ambapo amesema mkoa huo uko hatarini kugeuka jangwa na tayari vyanzo vingi vya maji vimeanza kukauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira unaosababisha ukame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa LINDI, GODFREY ZAMBI, amewataka watendaji wa kata na vijiji kuimarisha ulinzi wa maeneo ya misitu na maji na atakayeshindwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakati huo huo Mke wa Waziri Mkuu MARY MAJALIWA
ameiomba jamii ya watanzania kuwasaidia watoto wenye ulemavu wa ngozi.
Mama MAJALIWA ameyasema hayo wakati alipokwenda kutoa misaada kwa watoto wenye ulemavu huo katika kijiji cha MITOPE kilichopo wilaya ya RUANGWA Mkoani LINDI.
Share:

Viongozi wa Mila wa jamii ya Wamasai wametakiwa kusuluhisha na kutatua migogoro ya ardhi


Viongozi wa Mila wa jamii ya Wamasai wametakiwa kusuluhisha na kutatua migogoro ya ardhi,maeneo ya malisho pamoja na wizi wa mifugo ili kuepusha uvunjifu wa amani na kuzorota kwa maendeleo kunakosababishwa na migogoro hiyo.
Hayo yameelezwa na Wazee wa Mila Peter Toima na Lemamiye Shininii wakati wa sherehe za kuhama rika ambao Maelfu wa vijana kutoka Wilaya ya Simanjiro wanahamia rika la wazee na kukabidhiwa wajibu wa kuwa wasuluhishi katika jamii.
Wazee hao Walisema kuwa jukumu la kutatua migogoro linapaswa kufanywa na Wazee hao wapya na kuepuka kuitwisha serikali mzigo mkubwa wa migogoro ambayo wangeweza kuitatua .
Kwa upande wao Vijana waliohama rika na kuingia rika la wazee Oreka Mlolo na walisema kuwa kazi kubwa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha kuwa jamii inaishi kwa amani ,kudumisha umoja na ushirikiano ambazo ni tunu muhimu kwa jamii ya Wamasai.
Mmoja wa Kinamama ambao Waume zao wameama rika Loema Thadey alisema kuwa mila hiyo hutumika kupima uaminifu wa Wanandoa iwapo Mwanamke anachepuka basi anaweza kupoteza maisha.
Jamii ya Wamasai ni jamii yenye tamaduni yenye nguvu iliyodumu kwa muda mrefu na kuenziwa licha ya changamoto ya utandawazi uliomeza tamaduni nyingi za Kiafrika na kuleta utamaduni wa nchi za Magharibi.
Share:

Wanaopata mikopo ya elimu ya juu ni wenye vigezo na uhitaji tu


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na mafunzo ya ufundi, imesema mikopo inayotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu inatolewa kwa wahitaji kwa kuzingatia bajeti iliyopo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, naibu waziri, Bi Stella Manyanya amesema hali ya baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo inatokana na wao kutokidhi vigezo.
“Tunaangalia wale wahitaji na uhitaji huo lazima uhakikishwe vizuri, kwasababu kuna watu wengine unakuta wanadiriki hata kusema uongo. Tumeshayashuhudia hayo sana. Mimi nina uhitaji wakati ana fahamu fika anataka tu fedha kwaajili ya kulewea pombe, anataka tu fedha kwaajili ya kutembelea,anataka anunue TV,mwingine anaamua kujenga sasa hivi akiwa shuleni, sasa hatuwezi kwenda katika sura hiyo,lazima tuthibitishe kwa kina,kwamba huyu kweli ni mtu mwenye uhitaji na mwenye uhitaji aweze kusaidiwa,bila kujali kwamba huyu yuko wapi,lakini tunaenda hatua kwa hatua,”alisema.
“Lakini ninaposema wenye uhitaji lazima tukubaliane kwamba kama sheria inavyosema kwamba pamoja na uhitaji si rahisi kwamba wote kabisa wakapata,lazima kuna wengine watajikuta wamekosa,lengo ni kwamba tumesaidia kwa kadri inavyowezekana, tumesaidia kwa jitihada zetu zote,”aliongeza.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa bodi ya mikopo ya elimu ya juu, Abdurazak Badu, amesema awamu ya kwanza ya mikopo imeanza kutolewa kwa wanafunzi waliokidhi vigezo ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 80 kwaajili ya mikopo hiyo huku serikali ikiwasisitiza wanafunzi hao kutumia mikopo hiyo kwa lengo lililokusudiwa.
Share:

Barcelona, Man City kukipiga leo


BARCELONA, HISPANIA
USIKU wa Ulaya unatarajia kuendelea leo kwa michezo nane kupigwa katika viwanja mbalimbali, huku mchezo unaotarajiwa kugusa hisia za watu wengi ni kati ya Barcelona ambao watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Manchester City.
Mbali na kuwepo kwa michezo mingi leo, dunia itasimama kwa muda kwa ajili ya kuutazama mchezo huu ambao ni wa kiufundi.
Makocha wa timu hizo wote waliwahi kuitumikia klabu ya Barcelona wakiwa kama wachezaji, lakini leo hii wanakutana na kuonesha ufundi wao, Pep Guardiola akiwa kocha wa Manchester City, huku Luis Enrique akiiongoza Barcelona.
Guardiola alikuwa na mchango mkubwa akiwa na klabu ya Barcelona tangu mwaka 2008 hadi 2012 alipojiunga na Bayern Munich ya nchini Ujerumani, aliipa mafanikio makubwa ambayo yatakumbukwa kwa kiasi kikubwa.
Katika mchezo uliopita wa klabu bingwa, Man City walikutana na Celtic na kutoka sare ya 3-3, leo hii wanakutana na Barcelona ambayo mchezo wao uliopita waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Monchengladbach.
Hata hivyo, Pep Guardiola ameshindwa kuzuia hisia zake kwa klabu ya Barcelona ambapo ameweka wazi kuwa mchezo huo utakuwa mgumu sana kutokana na ubora wa wapinzani wake.
“Najua uwezo wa klabu ya Barcelona, ninaamini mchezo utakuwa mgumu sana ubora wa wenzetu upo juu tofauti na sisi, lakini chochote kinaweza kutokea kwenye soka.
“Naweza kusema kuwa Barcelona ni kama mashine, kuna wachezaji watatu ambao ni hatari katika safu ya ushambuliaji,” alisema Guardiola.
Kwa upande wa Enrique, alisema hajazungumza na Guardiola, lakini anaamini mchezo huu utakuwa wa aina yake kwa kuwa Guardiola ana uwezo mkubwa.
Michezo mingine ambayo itapigwa leo ni pamoja na Napoli itakayopambana na Besiktas, Arsenal itacheza na Ludogorets, wakati huo FC Rostov wakipambana na Atletico Madrid, Dynamo Kyiv dhidi ya Benfica, PSG watacheza na FC Basel, Monchengladbach watacheza dhidi ya Celtic na Bayern Munich watacheza na PSV Eindhoven.
Share:

Yanga, Azam vita nyingine


BAADA ya Yanga na Azam kupata sare tasa mchezo uliopita. Leo zina kazi nyingine ngumu ya kutafuta pointi tatu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania bara itakayochezwa viwanja tofauti.
Yanga itakaribishwa na Toto Africans kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, wakati Azam FC itakuwa na mchezo mgumu utakaochezwa kuanzia saa moja jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Timu zote hazina matokeo mazuri yaliyopita, kila mmoja ni lazima itacheza mchezo wa kumaliza hasira ilimradi kupata pointi ambazo zitawasogeza karibu na kinara wa ligi, Simba inayoongoza kileleni mwa msimamo kwa pointi 23.
Bila shaka kupona kwa mshambuliaji Amis Tambwe aliyekuwa majeruhi na kurudi kwa kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima aliyekuwa na matatizo ya kifamilia, huenda kukaendelea kuleta matumaini mapya ya kupata ushindi katika mchezo huo.
Wachezaji watakaokosekana katika mechi ya leo ni Juma Abdul aliyeumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam FC, Malimi Busungu aliyedaiwa kuwa ana matatizo ya kifamilia wakati Ali Mustafa anauguza jeraha.
Yanga na Toto ni timu ambazo zimekuwa zikihusishwa kuwa na uhusiano wa karibu na hasa kwa vile viongozi wa Toto kudaiwa kuwa na mapenzi na timu hiyo ya Jangwani. Mechi ya msimu uliopita baadhi yao walijiweka pembeni mpaka baada ya mechi hiyo wakidai kuwa Yanga damu, hali iliyosababisha baadhi yao kusimamishwa uanachama.
Lakini mchezo wao hautakuwa rahisi kwa kila mmoja, hasa kwa Toto Africans ambayo imetoka kufungwa na Majimaji mabao 2-1. Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ikiwa na pointi 15, kukiwa na tofauti ya pointi nane dhidi ya vinara wa ligi hiyo Simba hivyo, kwa vyovyote wanahitaji ushindi kama kweli wanataka kuwa katika mbio za kutetea taji lao.
Toto, msimu huu umekuwa mbaya kwao, baada ya kucheza michezo 10, ikishika nafasi ya pili kutoka mwisho kwa pointi nane, baada ya kushinda michezo miwili, sare mbili na kupoteza sita. Mechi nyingine itakayochezwa leo ni Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.
Timu hiyo ya Chamazi imetoka kufanya vibaya katika michezo mitatu iliyopita, ikilazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Yanga, ikifungwa na Stand United bao 1-0 na sare dhidi ya Ruvu Shooting 2-2. Bila shaka kutokana na kiwango bora katika mechi yao iliyopita, huenda wakaendeleza mapambano na kuhakikisha wanashinda.
Azam FC inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 12 katika michezo tisa. Inakutana na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15 katika michezo 10. Hautakuwa mchezo rahisi kwa kila mmoja, kutokana na ubora wa kila timu. Ruvu Shooting inaikaribisha Mwadui kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Maafande hao hawako vibaya sana wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 13 katika michezo tisa waliyocheza. Mwadui inashika nafasi ya tatu kutoka mwisho kwa pointi tisa baada ya kushinda michezo miwili kati ya tisa, mitatu ikitoka sare na kupoteza minne. Pia, Ndanda inaikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Timu hii mara nyingi huwa haikubali kufungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, iko radhi ishinde au kutoka sare, Mbeya City itakuwa na kazi nzito. Timu zote zimecheza michezo 10, zikivuna jumla ya pointi 12 kila mmoja, City ikishika nafasi ya tisa na Ndanda ya 10 kwenye msimamo.
Stand United inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikikimbizana na Simba, kwa tofauti ya pointi tatu, wao wakiwa na pointi 20. Leo itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya kumenyana na Prisons inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 1. Mechi ya wawili hawa huwa haitabiriki na leo kila mmoja anahitaji matokeo.
African Lyon itakuwa mwenyeji wa Majimaji. Licha ya Majimaji kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Toto bado inaendelea kushika mkia ikiwa na pointi sita. Bila shaka kama inataka kujikomboa ni lazima ipambane kujiokoa ilipo kwa kushinda mechi zake. Lyon inahitaji kushinda bado ipo na pointi 10 katika nafasi ya 12.
Share:

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga


RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Emmanuel Mkumbo siku moja baada ya kufikishwa mahakamani kwa makosa ya usalama barabarani pamoja na kutishia kumuua kwa bastola askari wa usalama barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia Oktoba 18, 2016.
“Uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga atakayejaza nafasi ya Emmanuel Mkumbo utafanywa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu.
Julai 7, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya (DC) 137 za Tanzania Bara.
Katika uteuzi huo uliotangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mussa Iyombe, kati ya wakurugenzi wote 185 walioteuliwa, 65 wameteuliwa kutoka orodha ya wakurugenzi wa zamani na 120 ni wakurugenzi wapya, akiwamo Mkumbo aliyepangiwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.
Juzi, Mkumbo (41) alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumtishia kumuua kwa bastola askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo pamoja na kuvunja sheria za usalama barabarani.
Mkumbo, ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani na alisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Sunday Hyera, akisaidiana na Ediga Bantulaki mbele ya Hakimu Agripinas Kimanze.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao wa serikali, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kesi mbili, ya kwanza ikiwa ni kesi ya jinai kifungu cha 226 ya mwaka 2016 na ya pili ni kesi ya Usalama Barabarani Kifungu cha 222.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 15, mwaka huu, eneo la Mkambarani Wilaya ya Morogoro katika barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam wakati akiendesha gari aina ya Toyota Pajero yenye namba za usajili T 845 CTJ.
Kosa la kwanza linalomkabiri Mkurugenzi Mtendaji huyo ni kutishia kumuua kwa bastola askari aliyejulikana kwa jina la Koplo Titunda, akiwa katika majukumu yake ya kikazi na makosa mengine ni kuendesha gari lenye namba T845 CTJ aina ya Toyota Pajero bila ya kuwa na leseni na kuendesha gari bila bima.
Hyera alidai kuwa makosa mengine ni mwendo kasi katika eneo lililoruhusiwa kuendesha mwendo wa spidi 50 kwa saa, lakini alivuka na kufikia 85, kugoma kupeleka gari kituo cha Polisi na kuendesha bila kuwa na uangalifu barabarani.
Mtuhumiwa huyo alikana makosa hayo na kuachiwa kwa dhamana, huku kesi yake ikitarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo Oktoba 31, mwaka huu, Hata hivyo, jitihada za waandishi wa habari kupata picha ya mtuhumiwa hazikufanikiwa baada ya askari kumziba mtuhumiwa kwa koti pamoja na kofia aina ya pama na kumuingiza katika gari aina ya Toyota na kutokomea naye.
Share:

Panya Road azinduka akiwa Mochwari


MTOTO aliyetambuliwa kwa jina la Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi cha uhalifu cha ‘panya road’ amezinduka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Ernest, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na mkazi wa Buza, anayedaiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi hicho, alidhaniwa amekufa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuwaibia mali zao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna vijana watatu wamekufa katika eneo la Mbagala na baada ya kufika eneo la tukio waliwakuta vijana hao wakiwa na hali mbaya.
Kamanda Muroto alimtaja mmoja aliyejulikana kwa jina la Kelvin Nyambocha (14) kuwa alikufa baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi na kwamba kabla ya mauti kumkuta alifuatana na wenzake kwa ajili ya kwenda kuangalia tamasha la muziki wa Singeli lililofanyika Mbagala Zakhem.
Kijana mwingine Selemani Hamis (16), mkazi wa Kilingule, alifariki akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali ya wilaya Temeke.
“Wakati watu wanarudi kutoka katika tamasha hilo, kundi la vijana hao walianza kuwavamia watembea kwa miguu na kuanza kuwaibia mali zao na ndipo wananchi waliwakamata hao watatu na kuanza kuwapiga,” alisema Kamanda Muroto.
Alifafanua kuwa Ernest alipigwa hadi kuzimia na wananchi hao walijua kuwa amekufa ambapo alipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo kuwekewa namba na kuingizwa kwenye jokofu.
“Wakati mwili wake umewekwa chini kabla ya kuingizwa kwenye jokofu, alipumua na kuzinduka na kuonekana kuwa bado yupo hai hali iliyosababisha kupelekwa chumba cha uangalizi maalumu wa madaktari,” alisema.
Kamishna Muroto alisema baada ya kupata fahamu na afya yake kutengemaa alihojiwa na kuwataja wenzake 10 ambao yuko nao katika kundi moja.
Alisema kijana mwingine fundi magari aitwaye Faraji Suleiman (19) mkazi wa Buza Kwa Rulenge, hali yake ni mbaya na amelazwa katika Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Alisema Polisi kupitia Sheria ya Watoto ya Mwaka 2009 kifungu 7/9, wazazi wana wajibu wa kuhakikisha mtoto anakuwa chini ya uangalizi wao, hawawekwi kwenye mazingira yatakayowasababishia madhara ya kimwili pamoja na kisaikolojia.
Alisema kuwa jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anakua kwenye malezi bora na sio kumuacha kwa walimwengu.
Aidha, alitoa mwito kwa mzazi yeyote kumsimamia vyema mtoto wake na kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 kifungu cha 14 na kwamba atakayeshindwa kutekeleza hayo atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atafungwa miezi 6 au kulipa faini ya Sh milioni tano.
Alisema kwa mazingira waliyokutwa watoto hao, wazazi wao ni watuhumiwa kwa kukiuka sheria hiyo ya watoto.
Awali taarifa ya Polisi, Temeke ilieleza kuwa inawashikilia vijana 16 wanaodaiwa ni wa kundi la uhalifu la ‘panya road’ liitwalo ‘taifa jipya’ kwa kuhusika kuwavamia watu kwenye tamasha la kuinua vipaji, la Oktoba 15 mwaka huu.
Share:

YouTube

Blog Archive

Pages

Our Facebook Page

Hali ya Hewa

Waliotembelea